Uchunguzi Wa Matumizi Ya Kiswahili Katika Ufunzaji Na Ujifunzaji Wa Shule Za Chekechea Katika Manispaa Ya Webuye, Kenya

IKISIRI

Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa ni kuchunguza matumizi ya Kiswahili katika

ufunzaji na ujifunzaji wa shule za chekechea. Utafiti ulifanywa katika Manispaa

ya Webuye katika Wilaya ya Bungoma Mashariki, Mkoani Magharibi nchini

Kenya. Sampuli ya watafitiwa iliteuliwa kwa kutumia mbinu za mfumo sahili na

njia nasibu sahili. Idadi ya wasimamizi 19, walimu 19 na wazazi 19 wa shule za

chekechea walikuwa sehemu ya sampuli.

Data ilikusanywa kupitia hojaji, masaili na kiongozi cha uchunzaji. Data

ilichanganuliwa kiidadi na kimaelezo. Michoro, chati na grafu zilitumiwa

kuwasilisha data iliyokusanywa, utafiti uliongozwa na nadharia ya uamilifu ya

Halliday (1970). Nadharia inafafanua kuwa lugha ndiyo nguzo muhimu katika

ufunzaji na ujifunzaji.

Utafiti uligundua kuwa lugha ya Kiingereza na lugha ya Kienyeji zilitumika katika

muktadha mmoja na lugha ya Kiswahili. Pia ilifichuliwa kuwa hakukuwa na

nyenzo na vielelezo katika lugha ya Kiswahili. Vilevile hakukuwa na maandalizi

ya semina katika matumizi ya lugha ya Kiswahili. Utafiti ulifichua kuwa wazazi

wengi wa chekechea hawakuunga mkono matumizi ya lugha ya Kiswahili. Japo

kulikuwa na vikwazo, Kiswahili ndiyo lugha iliyokuwa maarufu katika shule za

chekechea. Mtafiti anapendekeza kuwa jumuiya nzima ya chekechea izingatie

sera rasmi ya lugha ambayo inasisitiza matumizi ya lugha sambazi.

Lugha ya Kiswahili inastahili kuimarishwa, kukuzwa kama lugha ya kufundishia

katika shule za chekechea za miji. Iwapo ni lazima lugha nyingine kutumika, ni

sharti iwe katika miktadha tofauti. Jumuiya nzima ya chekechea inapaswa

kuunda nyenzo na vielelezo vyenye maandishi katika lugha ya Kiswahili. K.I.E

ipange semina juu ya matumizi ya lugha ya Kiswahili, kwa sababu walimu

watavumbua mikakati mipya itakayoendeleza lugha ya Kiswahili katika shule za

chekechea.