Athari Ya Matumizi Ya Mafumbo Na Tamathali Za Semi Katika Nyimbo Za Ngoma Ya Puuo Kwa Wazanzibari

IKISIRI

Kazi hii imedhamiria kufafanua athariya matumizi ya mafumbo na tamathali za semi zinazojitokeza katika nyimbo zinazoimbwa katika muktadha wa uganga wa puuo. Lugha inayotumika katika nyimbo hizo huwa teule na yenye ukwasi mkubwa katika utumiaji wa mafumbo na tamathali, kama vile ishara, methali, taswira, taashira, tashbiha na tashhisi. Aidha, utafiti huu umelenga kubainisha athari zinazojitokeza kutokana na matumizi ya mafumbo na tamathali za semi kwa jamii ya Wazanzibari.

Utafiti umeongozwa na Nadharia ya Semiotiki kwa kuzingatia mihimili yake katika kutafsiri ishara za kimafumbo na kitamathali zilizojitokeza katika nyimbo za ngoma ya puuo.Puuo ni aina ya ngoma ya uganga wa jadi ambayo hufanyika kwa baadhi ya jamii ya Wazanzibari ikiwa kama ni sehemu ya tiba kwa baadhi ya maradhi. Utamaduni huo upo na unaendelea kukua. Utafitiumegundua kuwepo kwa ukizani wa kimaana, ujumbe na dhima katika nyimbo za puuo kwa kupitia mitazamo na kauli za wasailiwa. Kwa hivyo, utafiti huu umetoa mchango katika kipengele cha fasihi simulizi kwani, tafiti zinazoelezea nyimbo za uganga wa jadi ni kidogo katika visiwa vya Zanzibar.

Data zimekusanywa uwandani katika kijiji cha Umbuji na Dunga, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar. Udurusu wa maandiko katika maktaba umesaidia kupata maelezo ya jinsi ya kutumia mafumbo na tamathali katika muktadha wake. Aidha, mbinu ya usaili, ushuhudiaji na udurusu wa matini umetumika katika kukusanyia data. Data zilichanganuliwa kwa kuzingatia malengo ya utafiti pamoja misingi ya Nadharia ya Semiotiki. Mwisho, matokeo ya utafiti huu yamewasilishwa kwa njia ya maelezo.