Korasi Katika Tamthiliya Ya Kiswahili: Mifano Toka Tamthiliya Teule Za Ebrahim Hussein, Emmanuel Mbogo, Na Frowin Nyoni

IKISIRI

Utafiti huu ulihusu Korasi katika Tamthiliya ya Kiswahili: Mifano toka Tamthiliya

Teule za Ebrahim Hussein, Emmanuel Mbogo, na Frowin Nyoni. Dhana ya korasi

imetumiwa ikimaanisha matendo, fikra au maneno ya kisanaa ayatoayo mtu au kikundi

cha watu katika kitendo cha kisanaa kwa njia ya uimbaji, uradidi, nathari na kuambatana

na vitendo. Matumizi ya mbinu hii ya korasi hayajatafitiwa wala kuhakikiwa vya

kutosha katika Fasihi ya Kiswahili. Hali hii inakifanya kipengele hiki kutojulikana sana

na wasomi na wanajamii wengi. Tamthiliya za waandishi teule zilizotafitiwa ni Kwenye

Ukingo wa Thim, Ngoma ya Ng’wanamalundi na Mabepari wa Bongo.

Utafiti huu ulifanyika maktabani kwa kiasi kikubwa. Vilevile mtafiti alifanikiwa

kuzungumza na wataalamu mbalimbali wa fasihi ili kupata mawazo komavu kuhusiana

na mada. Uchanganuzi wa data na uwasilishaji wa matokeo ya utafiti uliongozwa na

Nadharia ya Mwitiko wa Msomaji kupitia nguzo yake kuu ya uhuru wa msomaji wa

kupata maana kutokana na uzoefu wake.

Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa kipengele cha korasi hutumika katika tamthiliya

kwa malengo mahususi na wala si kwa bahati nasibu tu. Mchango mpya ulioibuliwa na

utafiti huu ni: Kwanza, ni kupanua ufafanuzi wa dhana ya korasi. Pili, ni kuonyesha

nafasi ya korasi katika tamthiliya, hususani katika tamthiliya za waandishi teule. Tatu,

ubainishaji na uchambuzi wa dhima za korasi ambazo ni kutambulisha onyesho,

kuunganisha onyesho moja na jingine, kuwasilisha dhamira, kudhihirisha ujumi, kujenga

taharuki, kuleta ucheshi na kufunga onyesho. Hivyo, korasi hutumika kama nguzo katika

ujenzi na uendelezaji wa tamthiliya.