Mabadiliko Ya Vionjo Vya Kiuandishi Katika Riwaya Ya Kiswahili: Ulinganisho Wa Riwaya Za Shaaban Robert Na Said A. Mohamed

IKISIRI

Tasnifu hii inahusu Mabadiliko ya Vionjo vya Kiuandishi katika Riwaya ya Kiswahili.

Utafiti ulijigeza katika kulinganisha na kulinganua mabadiliko hayo katika riwaya za

Shaaban Robert na Said A. Mohamed. Neno vionjo katika tasnifu hii limetumika kama

hali ya kimajaribio au mwondoko wa utanzu fulani wa Fasihi kutoka sura iliyozoeleka

kwenda sura mpya ambayo haijazoeleka. Mtafiti ameamua kuchunguza mabadiliko ya

vionjo vya kiuandishi katika riwaya ya Kiswahili kwa sababu, kwa kiasi kikubwa bado

dhana hii ya mabadiliko ya vionjo vya kiuandishi haijafanyiwa uchunguzi.

Utafiti ulifanyika maktabani na uwandani. Maktabani tuliyadurusu mapitio mbalimbali

kama vile majarida, tasnifu, tahakiki, makala na vitabu. Uwandani tulitumia mbinu ya

mahojiano ili kupata data za utafiti wetu. Utafiti ulitumia nadharia ya uhalisia ambayo

humtaka mtunzi kutunga kwa kuzingatia suala la wakati pamoja na kujua historia ya jamii

husika. Mabadiliko haya katika riwaya ya Kiswahili yanazingatia pia vitu hivyo.

Matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa uandishi wa riwaya ya Kiswahili umebeba

mabadiliko kadhaa katika uandishi wake. Mabadiliko haya katika vionjo vya kiuandishi

yanachangiwa sana na vitu kama vile mabadiliko ya kijamii (historia za jamii),

umajaribio, ongezeko la wasomi na hata maendeleo ya sayansi na tekinolojia kwa kiasi

kikubwa. Mchango mpya wa tasnifu hii ni kuonesha vionjo vinavyotumiwa na waandishi

mbalimbali katika utunzi hasa katika riwaya ya Kiswahili.